AdSense

Saturday 21 March 2015

On 03:51 by Unknown in    No comments
 
SERIKALI imewasilisha bungeni muswada wa sheria ya usimamizi wa maafa ambao unalenga kuanzisha chombo kinachojitegemea ambacho kitashughulikia maafa.
 
Nia ni kupunguza urasimu unaochelewesha maamuzi ya kujiandaa, kupunguza athari, kukabili maafa na kurejesha hali baada ya maafa kutokea.
 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Jenista Mhagama aliliambia Bunge kuwa sheria inayopendekezwa itawezesha uwepo wa mfumo mzuri wenye kukidhi weledi wa menejimenti ya maafa.
 
Alisema mfumo huo unaoendana na wakati kwa kuzingatia hali halisi ya mabadiliko ya tabia nchi pamoja na matakwa ya maridhiano ya kikanda na kimataifa kuhusu menejimenti ya maafa.
 
Alisema muswada huo utaruhusu kuanzishwa kwa wakala unaojitegemea wa menejimenti ya maafa utakaokuwa chini ya Waziri Mkuu.
 
Alisema wakala huo utakuwa ni kitovu cha taifa cha kuratibu masuala ya menejimenti ya maafa na shughuli zake zitaratibiwa na baraza ambalo litakuwa na jukumu la kusimamia utendaji wa wakala na kumshauri waziri mkuu.
 
Alisema lengo la kuwasilishwa kwa muswada huo ni kutokana na sheria ya uratibu wa misaada ya maafa ya mwaka 1990 inalenga zaidi katikakukabili, badala ya kuzuia na kupunguza athari zinazotokana na maafa.
 
Alisema sheria hiyo inatekelezwa kwa kutumia miundo ya kawaida ya wizara na idara za serikali ambayo haizingatii dharura ya maafa.
 
“Kwa msingi huo, Serikali imeona ni vema kufanya mapendekezo ya mabadiliko ya mfumo mzima wa menejimenti ya maafa nchini kwa kutumia muswada huu unaopendekeza sheria mpya,” alisema Mhagama.
 
Aliongeza kuwa upungufu wa sheria ya sasa ni kwamba haitilii mkazo suala zima la mfumo wa menejimenti ya maafa na kubaki kuzingatia hatua moja ya utoaji wa misaada tu pindi maafa yanapotokea.
 
Sheria ya sasa pia haijatamka kuanzishwa kwa kituo cha kufuatilia mwenendo na uratibu wa maafanchini.
 
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala Jason Rweikiza alisema muswada huo umepelekwa bungeni katika muda muafaka kwani nchi imekuwa ikikumbwa na majanga ya aina mbalimbali na hivyo kusababisha maafa kwa jamii ikiwemo kupoteza maisha ya watu na mali zao.
 
Alisema kamati yake inaona umuhimu na haja kubwa ya utungwaji wa sheria hiyo ili kuweka mfumo mzuri wa madhubuti utakaokidhi weledi wa menejimenti ya maafa nchini unaoendana na wakati.
 
Kwa upande wake, msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema muswada huo ni mojawapo ya mifano mbaya ya kutunga sheria bila kuzingatia masharti ya katiba ya nchi wala kuangalia uwepo wa sheria nyingine zinazoshughulikia masuala hayo.
 
Lissu alisema muswada huo utapoka mamlaka ya kikatiba na kisheria ya rais katika kushughulikia mambo ya maafa kwa sababu kikatiba ni rais pekee mwenye mamlaka ya kutangaza hali ya hatari katika nchi.
 
Alisema maafa na majanga ni baadhi ya mambo ambayo yanaangukia kwenye sheria ya hali yahatari.
 
Alisema licha ya kuwa kwenye katiba hakuna neno maafa ambalo limetumika kwenye muswada huo, lakini maana ya neno hilo ni hatari ya dhahiri na kubwa, tukio la hatari, tukio la balaa au baa ya kimazingira na hali ya kuvurugika kwa amani ya jamii. Wabunge waliupitisha muswada huo.

0 comments:

Post a Comment