AdSense

Friday, 20 March 2015

On 18:44 by Unknown in    No comments
 
Pofesa Ibrahim Haruna Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf) siyo mtu wa kutiliwa shaka kuhusu ‘madini’ aliyonayo kichwani. Ni msomi aliyebobea kwenye masuala ya uchumi duniani.
 
Amezaliwa Juni 6, 1952, katika kijiji cha Ilolangulu mkoani Tabora. Safari ya elimu iliyompa uprofesa aliianza mwaka 1959, akisoma elimu ya awali na msingi katika shule ya Sikonge.
 
Baadaye akajiunga na Sekondari ya Tabora Boys, akaenda Pugu Sekondari, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kisha kupaa ng’ambo chuo cha  Stanford nchini Marekani alikotunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya uchumi.
 
Safari ya elimu ya Profesa Lipumba ni ndefu lakini ni yenye mafanikio makubwa. Sina shaka ni kutokana na uwezo wa kimasomo aliokuwa nao mhusika na mvuto miongoni mwa wanafunzi wenzake ambapo aliukwaa uongozi karibu kila awamu ya masomo aliyojiunga nayo.
 
Akiwa shule ya msingi alikuwa kiranja, Tabora Boys akachaguliwa kuwa Mweka Hazina wa Umoja wa Vijana. Pugu Sekondari alikuwa mjumbe wa Kamati ya Umoja wa Vijana, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana, akahitimisha safari yake ya kimasomo wa kuwa Rais wa Kwanza wa Umoja wa Vijana wa chuo cha Stanford.
 
Kwa mtiririko huu wa uongozi, Profesa Lipumba ana nyota ya uongozi hivyo haliwezi kuwa jambo la kutilia shaka unaposikia kuwa chama chake kimemteua kuwa mgombea urais anayetafuta tiketi ya uwakilishi wa muungano ya vyama za kisiasa vya upinzani nchini (Ukawa).
 
Sifa  za  Kuwakilisha  UKAWA  Urais  2015  Anazo?
Wafuasi wake ndani na nje ya chama wanamuona anafaa. Hata mwenyewe amejinasibu mara nyingi kuwa ni mtu asiyejitilia shaka katika kubeba dhima ya uongozi wa nchi.
 
Pengine ni kwa sababu amekuwa kiongozi mzuri katika maisha yake. Maana mbali na maisha ya shule niliyoeleza, Profesa Lipumba amewahi kuwa msaidizi wa rais wa masuala ya uchumi nchini kati ya mwaka 1991-1993, wakati huo Rais wa Jamhuri alikuwa Ali Hassan Mwinyi.
 
Mbali na kazi hiyo ambayo ameifanya ikulu, ana hazina ya elimu ya uchumi ambayo ndiyo msingi wa matatizo ya nchini hivi sasa. Lulu ya elimu yake siyo tu imetambulika Tanzania kama nchi maskini inayohaha kujikwamua kiuchumi, la hasha! Hata taasisi na mashirika makubwa duniani yamepata kutumia ufahamu wake katika kujiendesha.
 
Profesa Lipumba amewahi kuwa mmoja wa washauri wa masuala ya uchumi wa Benki ya Dunia (WB), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Norway (NORAD), Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Denmark (DANIDA), Shirika la Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa la Sweden (SIDA), Dawati la Uchumi Mambo ya Nchi za Nje nchini Finland na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
 
Hayo ni kwa uchache, lakini kiongozi huyu amepata pia kushiriki katika utafiti wa  kibiashara wa nchi za Kusini mwa Afrika, amepata kuwasilisha mada Shirika la Fedha la Dunia (IFM) kuhusu namna ya kuzisaidia nchi maskini ikiwemo Tanzania na kisha kutayarisha vigezo kuhusu utambuzi wa nchi maskini zaidi duniani.
 
Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Bunge wa Cuf wakati akimtangaza Profesa Lipumba kuwa ni mgombea wao wa urais kupitia Ukawa alisema hawana shaka juu ya sifa za mwenyekiti huyo kupeperusha bendera ya upinzani kuwania urais na akasisitiza kuwa vigezo vikitazamwa hakuna wa kumlinganisha naye.
 
Naam, hata mimi na wengineo tunapotazama rekodi, elimu na uzoefu wa Profesa Lipumba hatuna cha kubisha zaidi ya kusema anafaa sana kuwa rais wa awamu ya tano.
 
Usomi  na  Rekodi  Vitamsaidia  Lupumba  Kuwa  Rais  2015?
Sitarajii jibu likawa ndiyo kwa sababu Lipumba ameshaonja joto la jiwe la uchaguzi mkuu wa rais kwa miaka 20, akaangukia pua!
 
Mwaka 1995, alipojitosa mara ya kwanza katika kinyang’anyiro cha uchaguzi Profesa Lipumba alipigwa mwereka na Benjamin Mkapa ambaye hakuwa na kiwango kikubwa cha elimu.
 
Nakumbuka alishika nafasi ya tatu nyuma ya Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi (wakati huo) Augustino Mrema, ambaye moto wake wa siasa za upinzani ulikuwa mkali.
 
Mwaka 2000 Lipumba alirudi tena kwenye kinyang’anyiro dhidi ya Mkapa, akajitutumua mno na kushika nafasi ya pili. Wengi na hasa wafuasi wake waliamini kuwa kasi aliyokuwa nayo huenda ingekiwezesha chama chake kushika dola kwenye uchaguzi wa mwaka 2005. Haikuwezekana!
 
Alitimiza mwaka wa 20 kwa kurudi tena kwenye uchaguzi mkuu kuwania urais, mkononi mwake akiwa na usomi, rekodi na uzoefu wa masuala ya uchaguzi; hapo pia nyota haikuwaka!  2010, aliyeshinda akawa rais wa sasa, Jakaya Kikwete, akifuatiwa na Dk. Wilbroard Slaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na yeye akiambulia nafasi ya tatu. Waliomtangulia hawakuwa na sifa kama zake.
 
Profesa  Lupumba  Ataweza  Kukata  Kiu  ya  Urais  2015?
‘Maradhi ya kisiasa’ yaliyomdhoofisha kwenye uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi bado hayajatibika. Uzoefu wa ushindi katika nchi hii unategemea, pamoja na mambo mengine, nguvu ya chama cha mgombea.
 
Mwaka 1995, chama cha Cuf hakikuwa maarufu  ukilinganisha na NCCR-Mageuzi cha Mrema.  Matokeo hayakuleta miujiza, ushindi ulipangwa kulingana na nguvu ya vyama. Bila chama imara hujaeleweka bado; tatizo hilo halijatafutiwa tiba na Cuf.
 
Binafsi sijaona mapinduzi ya umaarufu; Cuf iliyokuwa chama kikuu cha upinzani imebaki kuwa mshiriki wa tatu.  Nachelea kuamini kuwa ndoto za Lipumba kuingia ikulu zinaweza kutimia 2015, ingawa kwa sehemu fulani malengo ya Ukawa kuunganisha nguvu yakitimia yanaweza kubadilisha matokeo.
 
Hata hivyo, hiyo inabaki kuwa imani kwa sababu  Chadema ambao ni washirika wakubwa wa Cuf nao wanatumaini la kumweka mgombea wao wakiamini umaarufu wa chama chao waliotoka nao kwenye uchaguzi uliopita wakiingia nao mwaka huu wataumalizia mkia wa CCM walioubakiza 2010 na hivyo kuingia ikulu.
 
Ikiwa ni hivyo, sioni uchu wa urais wa Lipumba aliodumu nao kwa miaka 20 kama unapata ‘nyama’ ya kutafuna mwaka huu! Pengine miujiza itokee maana wakati mwingine upepo wa siasa hugeuka.
 
Hapa ndipo ninapoona Ukawa wanafuata ‘mkono’ wa CCM unaoning’inia wakiamini huenda utaanguka wapate kitoweo; hii ni falsafa ya fisi kufuata mkono wa binadamu akiamini utaanguka autafune.
 
Kwa mbali naona Ukawa wanasubiri chama tawala wavurugane, wateue asiyefaa ili wao wapate kura za hasira za wafuasi wa CCM ambao hawataridhika na uteuzi wa mgombea waliyemtarajia kuwaletea mabadiliko.

0 comments:

Post a Comment